PSSSF YASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026
Dodoma, Juni 17, 2026
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), unashiriki katika Maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yanayoafanyika kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ameyafungua rasmi leo Juni 17, 2026.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akihutubia kwenye uzinduzi wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma Juni 17, 2026
Akizindua maonesho hayo, Waziri Kikwete amezungumzia Programu ya maboresho katika Utumishi wa Umma yenye mrengo wa kuwahudumia wananchi. Amesema Serikali itajikita katika mabadiliko ya fikra katika sekta ya Umma kwa utoaji wa huduma bora ambayo ni Ujumuishaji, ushirikishaji wa wananchi, Uongozi na uwajibikaji, Usimamizi wa rasilimaliwatu pamoja na mageuzi ya huduma kidijitali.

Afisa Utumishi PSSSF, Bw. Denis Kaitwa, (kulia), akimuunganisha mwanachama wa PSSSF, Bi. Rebeca Hoza na huduma ya PSSSF Kidijitali kupitia simu janja, alipotembelea banda la PSSSF kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma Juni 17, 2026
Akizungumzia ushiriki wa PSSSF kwenye maonesho hayo, Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi amesema Mfuko unatumia fursa ya maonesho hayo kuhudumia wanachama pamoja na wananchi na kuonesha mafanikio na maboresho yaliyofanywa na Mfuko. Aidha, amesema wanachama wanahamasishwa matumizi ya TEHAMA kupitia PSSSF Kiganjani na PSSSF Portal katika kupata huduma zote zitolewazo na Mfuko.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uendeshaji, PSSSF, Bw. Franklyn Boga (kulia) akimuelimisha mwanachama wa PSSSF, Bi. Sofia Kutona alipofika kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma viwanja vya Chinangali jijini Dodoma Juni 17, 2026.
"Kupitia PSSSF Kidijitali mwanachama na mstaafu ataweza kujihudumia yeye mwenyewe wakati wowote kupitia kompyuta au simu janja, na hii inaongeza uwazi na uwajibikaji," amesema Bw. Abdul

Picha ya pamoja ya watumishi wa PSSSF kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma Juni 17, 2026