DKT. NYANSAHO, DKT. MUNISI WASIFIA UBUNIFU WA TEKNOLOJIA BANDA LA PSSSF
Dar es Salaam, Julai 6, 2026
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Dkt. Eveline Munisi, wamepongeza ubunifu wa kiteknolojia unaotumiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika utoaji wa huduma kupitia Meza Janja (Smart Table).

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho (wa pili kushoto waliokaa), Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tnazania (JWTZ), Meja Jenerali Iddi Nkambi (wa kwanza kushoto waliokaa), Naibu Mkurugenzi wa Suma JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi (wa pili kulia waliokaa) na Mkurugenzi wa Fedha, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Bw. Ali Yakiti (wa kwanza kulia waliokaa) wakifurahia baada ya kupewa maelezo ya namna meza janja (Smart Table) inavyotoa huduma kidijitali kwenye banda la PSSSF kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendela kwenye Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Julai 6, 2026.
Viongozi hao walitoa pongezi hizo walipotembelea kwa nyakati tofauti banda la PSSSF ndani ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo walijionea namna Mfuko unavyotumia teknolojia za kisasa za kidijitali kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na wananchi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, na ujumbe wake, wakitembelea banda la Mfuko wa PSSSF Julai 6, 2026, ambapo walinaongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. Omega Ngole (kushoto).
Akiwa katika banda la PSSSF, Dkt. Nyansaho aliambatana na Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Iddi Nkambi, pamoja na Naibu Mkurugenzi wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Shija Lupi.
Ujumbe huo wa Dkt. Nyansaho ulipokelewa na Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Bw. Ali Yakuti, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. Omega Ngole, ambao walitoa maelezo kuhusu huduma mbalimbali za Mfuko na maboresho ya kidijitali yaliyowezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Baada ya kushuhudia namna Meza Janja inavyorahisisha utoaji wa huduma, Dkt. Nyansaho aliipongeza PSSSF kwa kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
"Hongereni sana. Mnafanya kwa vitendo mageuzi ya utoaji huduma kidijitali. Hiki nilichokiona kimenifurahisha sana na kinaonyesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi," alisema Dkt. Nyansaho.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Munisi, ambaye aliambatana na Kamishna wa Kazi nchini, Bi. Suzan Mkangwa, alitembelea banda hilo na kupokelewa na Afisa Mkuu wa Uhusiano wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi, aliyempa maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko pamoja na ubunifu wa Meza Janja unaowawezesha wanachama na wananchi kupata huduma kwa haraka, urahisi na ufanisi zaidi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Munisi alisema ubunifu huo unaonesha dhamira ya PSSSF ya kuendana na mapinduzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma za umma.
"Hongereni sana PSSSF kwa kuendelea kutoa huduma kwa kutumia teknolojia za kisasa. Ubunifu huu unavutia, unaongeza ufanisi na unarahisisha wananchi kupata huduma kwa haraka zaidi," alisema.

Mstaafu Bi. Margareth Onjari (kulia) akihudumiwa na Afisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bi. Mary Malilo, kwenye banda la Mfuko katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

Mkurugenzi wa TEHAMA, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Eric Kato (kulia), akimuelekeza Mstaafu Bw. Said Mohammed, namna ya kupata huduma za Mfuko kupitia PSSSF Portal kwenye simu janja, alipofika kujihakiki kwenye banda la Mfuko katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viweanja vya Julius Nerere jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Fedha, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Ali Yakiti (kushoto) akifurahia jambo na Mwanachama wa Mfuko huo Profesa Momole Kasambala, baada ya kumuhudumia katika Banda la Mfuko kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu, PSSSF imeendelea kuvutia mamia ya wananchi wanaotembelea banda lake kwa kuwasilisha huduma kupitia Meza Janja (Smart Table), teknolojia inayomwezesha mteja kupata huduma mbalimbali za Mfuko katika mazingira ya kisasa, rafiki na yenye kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.