Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
MFUKO WA PSSSF WACHANGIA MILIONI 10 KWA MATIBABU YA WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA NA MGONGO WAZI MOI

MFUKO WA PSSSF WACHANGIA MILIONI 10 KWA MATIBABU YA WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA NA MGONGO WAZI MOI

Management

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umechangia kiasi cha shilingi milioni 10 kusaidia matibabu ya watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).


Mbali na mchango huo wa fedha, baadhi ya watumishi wa mfuko huo pia walikabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu kwa watoto hao, ikiwemo miswaki, sabuni za unga, pampasi na maziwa, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuboresha ustawi wao wakati wa matibabu.


Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Juni 03, 2026, Meneja wa PSSSF kanda ya Temeke, Bi. Maria Lupondo, amesema mfuko huo umeguswa na mahitaji ya watoto hao na kuona umuhimu wa kushiriki katika kuwasaidia ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo wao na familia zao.

"Mchango huu unaakisi dhamira ya PSSSF ya kurejesha sehemu ya mafanikio yetu kwa jamii kwa kuwasaidia wenye uhitaji, hususani watoto wanaohitaji huduma maalumu za matibabu".


Kwa upande wake, Meneja wa Wagonjwa wa Ndani MOI, Magreth Kumpuni, ambaye alipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, aliushukuru mfuko wa PSSSF kwa moyo wa kujitolea na msaada walioutoa.

Amesema mchango huo utasaidia kuboresha huduma na mahitaji ya watoto wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo, huku akizitaka taasisi na wadau wengine kuendelea kushirikiana na MOI katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu ya kiafya


Meneja wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya MOI, Magreth Kumpuni akiongea wakati wa kupokea msaada wa shilingi milioni 10, uliotolewa na PSSSF kwa ajili ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi


Baadhi ya watumishi wa PSSSF wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa MOI katika hafla ya kupokea msaada wa shilingi milioni 10 pamoja na mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wa Hospitali ya MOI