Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
SEMINA YA ELIMU YA PSSSF YAFANYIKA JKCI TAWI LA KAWE

SEMINA YA ELIMU YA PSSSF YAFANYIKA JKCI TAWI LA KAWE

News
News

Dar es Salaam, Kawe, Julai 27, 2026.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendesha semina ya elimu kwa wanachama katika tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Kawe.

Semina hiyo iliwasilishwa na maafisa wa PSSSF, Mordgard Matern Lumbanga na Alfonsi Peter Francis, ambao walitoa elimu kuhusu mafao na huduma mbalimbali zinazotolewa na mfuko kwa wanachama wake. Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni pamoja na mafao yote yanayotolewa na PSSSF, huduma mbalimbali zinazopatikana kwa wanachama, pamoja na wajibu wa wanachama katika kuhakikisha taarifa zao zinakuwa sahihi na za wakati.

Daktari bingwa mbobezi wa moyo Dkt. Naki Kiroga kutoka Taasisi ya Jakaya Kikwete akifuatilia semina ya elimu kuhusu PSSSF iliyotolewa na Watumishi kutoka PSSSF hospitalini hapo.

Bw. Mordgard, walisisitizwa wanachama kuhakikisha taarifa zao binafsi pamoja na michango yao zinakuwa sahihi na zilizohuishwa wakati wote. Aidha, walikumbushwa kuwa mabadiliko yoyote ya taarifa, ikiwemo kubadilisha majina, kuongeza wategemezi kama watoto, au kufanya marekebisho mengine muhimu, yawasilishwe PSSSF kwa wakati ili kuwezesha mfuko kuwa na taarifa sahihi na kurahisisha upatikanaji wa mafao kwa wakati stahiki.

Kuhusu namna ya kuwasilisha madai, Afisa Matekelezo Mwandamizi wa PSSSF, Bw. Alfonsi Francis, alisema, asilimia kubwa ya shughuli za Mfuko zinatolewa kupitia mtandao, ambapo aliwaambia kupitia simu janja, Mwanachama anaweza kupata taarifa mbalimbali zinazohusiana na uanachama wake, kama vile taarifa za Michango, taarifa za Mafao, kuwasilisha Madai mbalimbali lakini pia kuhuwisha taarifa zake.

Bw. Mordgard Lumbaga Afisa matekelezo Mkuu kutoka PSSSF, akitoa elimu kwa watumishi wa Taasisi ya Moyo JKCI tawi la kawe.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa semina hiyo, Daktari bingwa wa Moyo na Mkuu wa Kliniki hiyo, Dkt. Johnsoton Kayandabila, aliishukuru PSSSF kwa kuwatembelea na kuwapatia semina hiyo.

" Kwa niaba ya taasisi ya JKCI, tunapenda kuwashukuru PSSSF kwa elimu hii kuhusu Mafao lakini pia umuhimu wa kuchangia katika Mfuko. Tumeona kuna manufaa baada ya kustaafu, kujifungua, kupata ulemavu au hata kifo, tunasema asanteni sana. " Alisema.