Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
PSSSF YAKABIDHI MIRADI YA MAJI SHULE MBILI DODOMA

PSSSF YAKABIDHI MIRADI YA MAJI SHULE MBILI DODOMA

News
News

04 Novemba,2026.

*Mradi kunufaisha zaidi ya watu 1000, bustani kuanzishwa kuboresha lishe

Na Mwandishi wetu

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishvi wa Umma (PSSSF) umekabidhi rasmi miradi miwili ya visima vya maji katika Shule ya Sekondari Kimaghai, Wilaya ya Mpwapwa, na Shule ya Msingi Uhuru, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za PSSSF kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na mazingira ya kujifunzia.

Picha ikionyesha Uzinduzi rasmi wa mradi wa maji katika Shule ya Sekondari Kimaghai A, kulia akiwa ni Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw, Dismas Pesambili na kushoto akiwa ni Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw Lulyaya Sayi.

Makabidhiano hayo yalifanyika tarehe 3 na 4 Novemba 2026, yakiongozwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi. Mradi wa Kimaghai ulipokelewa na Mkuu wa Shule, Bi. Eudia Medaa, na wa Uhuru ulipokelewa na Mkuu wa Shule, Bi. Agatha Mosha.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi wa Kimaghai, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Ally Akida, aliishukuru PSSSF kwa msaada huo akieleza kuwa kisima hicho kimetatua changamoto ya muda mrefu ya maji na kinatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 600, wakiwemo wanafunzi, walimu na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shule hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa (Kaimu), Bw. Ally Akida, akijumuika na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyalya Sayi, pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kimaghai A, Bi. Eudia Medaa, Afisa Mipango wa Wilaya, Bw, Dismas Pesambili, na viongozi wengine wakishuhudia uwepo wa maji yanavyopatikana kwa uhakika baada ya kukamilika kwa mradi huo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji katika Shule ya Sekondari Kimaghai A.

Katika makabidhiano katika shule ya Msingi Uhuru ya jijini Dodoma, Kaimu Afisa Elimu wa jiji la Dodoma, Bw. Yasin Mponda, aliipongeza PSSSF kwa kuthamini ombi la Shule ya Uhuru na kusema, “PSSSF imeacha alama kubwa katika Shule ya Uhuru. Pamoja na majukumu yake mengi, Mfuko umeamua kuthamini ombi letu na kutufanya tujione kuwa tunathaminiwa”.

Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw, Lulyaya Sayi, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya mji Dodoma Bw, Yasin Mponda, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru wakishuhudia uwepo wa maji kwa uhakika baada ya kukamilika kwa mradi huo katika Shule ya Msingi Uhuru.

Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Bi. Agatha Mosha, aliishukuru PSSSF na kueleza kuwa maji yamewezesha shule kuanzisha kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya kuboresha lishe ya wanafunzi. Pia alisema mradi huo utanufaisha Zaidi ya watu 500.

Akikabidhi miradi hiyo, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi, aliwataka wanafunzi, walimu na wananchi kushirikiana katika kutunza visima na miundombinu yake ili viendelee kutoa huduma kwa muda mrefu na kunufaisha hata vizazi vijavyo.

Picha ya pamoja ikionyesha Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Dodoma, Bw. Yassin Mponda, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Bi. Agatha Mosha, pamoja na watumishi, wazazi, na wanafunzi waliohudhuria katika uzinduzi wa mradi wa maji katika Shule ya Msingi Uhuru.

Miradi hiyo inaonesha dhamira ya PSSSF ya kushiriki katika kutatua changamoto za msingi zinazozikabili jamii, hususan upatikanaji wa maji safi na salama, huku ikiunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu na afya.