Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
PSSSF YAAGA SHIMMUTA 2026, NIDHAMU YASISITIZWA KUELEKEA 2027

PSSSF YAAGA SHIMMUTA 2026, NIDHAMU YASISITIZWA KUELEKEA 2027

News
News

Morogoro, Novemba 19, 2026

Na Mwandishi Wetu,

Si haba. Safari ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye Mashindano ya 56 ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) 2026 mkoani Morogoro imefika tamati leo, huku michuano hiyo ikiendelea kusaka washindi.

Mwanariadha wa PSSSF (namba 030) Bw. Adrian Kyara akipambana kwa kasi kwenye mbio za riadha za wazee kuanzia miaka 50 na kuendelea katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro katika Mashindano ya 56 ya SHIMMUTA 2026

Katika siku ya kuaga, wachezaji wa PSSSF walipambana kwa ushindani na nidhamu kubwa kwenye riadha (mita 5,000), mbio za wazee (mita 800), mbio za magunia (mita 100), bao, karata, drafti na pool table, japo matokeo hayakutosha kuuvusha Mfuko huo pendwa katika hatua inayofuata.

Wachezaji wa PSSSF Bw. Selemen Majingo akichuana katika mchezo wa bao katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro wakati wa Mashindano ya 56 ya SHIMMUTA 2026.


Mshiriki kutoka PSSSF Bi. Asia Msuya akipiga mpira kwa umakini kwenye mchezo wa pool table mkoani Morogoro wakati wa Mashindano ya 56 ya SHIMMUTA 2026

Meneja wa Rasilimaliwatu na Utawala, Bi. Glory Mboya, amewapongeza wachezaji kwa uzalendo, mshikamano na uwakilishi mzuri, akisema:

“Kwa niaba ya Uongozi na Idara inayosimamia watumishi, tunawapongeza watumishi walioshiriki mashindano ya SHIMMUTA kwa niaba ya Mfuko na tunaamini wametuwakilisha vizuri. Kutofika hatua ya mwisho kumetupa changamoto ya kujipanga vizuri zaidi ili tuweze kushiriki vyema mwaka unaokuja."

Meneja wa Rasilimaliwatu na Utawala wa PSSSF, Bi. Glory Mboya, akizungumza kwa niaba ya Kurugenzi ya Rasilimaliwatu na Utawala kuwapongeza wanamichezo wa mfuko huo kwa uwakilishi wao na kuwahamasisha kujipanga upya kwa ajili ya mashindano ya SHIMMUTA 2026 yanayofanyika mkoani Morogoro

Amewataka wasikate tamaa bali waendelee na mazoezi na mikakati mipya, akisisitiza kuwa uongozi upo tayari kutoa msaada na kuunga mkono mipango ya maandalizi ya mwakani.

Naye Meneja wa Utawala wa PSSSF anayesimamia michezo, Bi. Fatma Chondo, akiongea na wanamichezo hao alisema:

Meneja wa Utawala wa PSSSF anayesimamia sehemu ya michezo ndani ya mfuko, Bi. Fatma Chondo, akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya kambi na maandalizi bora baada ya kutembelea mazingira ya michezo na kuzungumza na viongozi wa klabu na makocha mkoani Morogoro wakati wa SHIMMUTA 2026

"Matokeo ya mwaka huu yametupa chachu ya kujipanga vizuri na yajayo yanafurahisha, lakini pamoja na mazoezi ni lazima kuwepo na nidhamu ya kambi na kufuata taratibu kama sehemu ya kazi kwa sababu michezo bila nidhamu haiendi,” amesema.