PSSSF NA TPA ZAFUNGUA PAZIA LA SHIMMUTA 2026 MOROGORO MBELE YA WAZIRI MKUU
Morogoro, Novemba 12, 2026.
Timu za michezo za PSSSF zilizoweka kambi mkoani Morogoro kwenye mashindano ya SHIMMUTA zimeapa kupambana ili kupeperusha bendera ya Mfuko ambapo leo imeshiriki mchezo wa ufunguzi katika Uwanja wa Jamhuri, ambapo mchezo wa kuvuta kamba kati ya PSSSF na TPA ndio ulioufungua pazia rasmi mbele ya mgeni rasmi, Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Kikosi cha mchezo wa kuvuta kamba cha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kikichuana vikali wakati wa mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya 56 ya SHIMMUTA katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amezitaka taasisi kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha wafanyakazi kushiriki michezo mahali pa kazi na kufanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha. Lengo hili linaenda sambamba na kuunganisha wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali ili kujenga mshikamano, kupunguza msongo wa mawazo na kukuza ustawi wa afya.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na kikosi cha mchezo wa kuvuta kamba (wanaume) cha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) mara baada ya mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya 56 ya SHIMMUTA dhidi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Hadi sasa, vikosi vyetu vimeanza mapambano kwa kujiamini ambapo kwenye kuvuta kamba, timu ya wanaume imeshinda mechi moja na kupoteza moja huku ikibakiza michezo miwili ya mwisho kesho na kesho kutwa kusaka nafasi ya kusonga mbele. Kwa upande wa mpira wa miguu, timu imepata ushindi mmoja, sare moja na kupoteza miwili.

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bi. Zaida Mahava, akiwa katika picha ya pamoja na wanamichezo ambao ni watumishi wa PSSSF baada ya ufunguzi wa mashindano ya 56 ya SHIMMUTA mkoani Morogoro.
Wakati huo huo, michezo ya jadi ikiwemo drafti, bao, karata na mbio za wazee inatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo wachezaji wako fiti chini ya makocha wao. Lengo la PSSSF ni kuhakikisha inamaliza katika nafasi nzuri kwenye michezo yote iliyosalia.