KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII YAIIPONGEZA PSSSF KWA UWEKEZAJI WA KLICL
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakiwa katika ziara ya kutembelea Kiwanda cha Ngozi cha kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL) kinachozalisha Bidhaa za Ngozi leo Machi 13, 2026 Mkoani Kilimanjaro.

Moshi, Machi 13, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeiagiza, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano kwa kushirikiana na PSSSF kuweka mikakati thabiti ya masoko ndani na nje ya nchi kwa bidhaa zinazozalishwa katika Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL). Hatua hii inalenga kuongeza mauzo na kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zinazalishwa kwa tija ili kukuza uchumi wa viwanda nchini.
Maagizo hayo yametolewa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika kiwanda hicho, ambapo wajumbe walipokea taarifa ya utendaji na kujionea mchakato wa uzalishaji.

Akitoa taarifa ya awali kwa Kamati hiyo, Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Deus Sangu, alibainisha faida kubwa zitokanazo na kuwepo kwa kiwanda hicho. Mhe. Sangu alieleza kuwa kiwanda kimekuwa nguzo muhimu katika kuzalisha ajira kwa vijana wa Kitanzania, huku kikisaidia kuongeza thamani ya ngozi zinazotolewa na wafugaji nchini badala ya kuziuza kama ghafi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chafu (Mb), amesisitiza kuwa Wizara haina budi kuwa na mipango ya kisasa ya masoko ili kuhakikisha bidhaa zinazotengenezwa KLICL zinapata wateja wa uhakika kwani ubora wa bidhaa pekee hautoshi kama hakuna juhudi za kuzitangaza ili kukiwezesha kiwanda kujiimarisha kifedha.

Kiwanda cha KLICL kinamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko PSSSF na Jeshi la Magereza Tanzania ambapo huzalisha bidhaa za ngozi kama viatu, mikanda na mikoba, kwa kutumia teknolojia ya juu ya utengenezaji na uongezaji thamani zao la ngozi kuchangia katika uzalishaji wa ajira.
