*Aridhishwa na hatua iliyofikiwa

* Aipongeza PSSSF kwa usimamizi

*KASHIMBA: Mradi utakamilika ndani ya miezi miwili

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameupongeza  Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa usimamizi mzuri na wa karibu katika mradi wa machinjio ya kisasa ya yaliyopo Nguru Hills, wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Majaliwa alisema hayo Agosti 14, 2021 alipotembelea mradi huo ambao   unamilikiwa na wanahisa watatu ambao ni Eclipse Investiment LLC hisa asilimia 46, PSSSF hisa asilimia 39 na kampuni ya Busara Investment LLP wenye hisa asilimia 15.

“Mimi nimeridhika na uwekezaji na hatua ya asilimia 85 iliyofikiwa ambayo nimepata taarifa kwa Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda, lakini pia Mkurugenzi mwekezaji wa PSSSF kwamba kufikia Septemba kiwanda hiki kitafanyakazi”. Alisema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakaty alipotembelea eneo la mradi wa machinjio ya Nguru Hills uliopo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Akizungumzia uwekezaji nchini, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema, “Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendelea kuwahamasiha wawekezaji na ametupa dhamana ya kusimamia kuhakikisha uwekezaji unakwenda vizuri, wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini kwenye sekta ya viwanda, kilimo na maeneo mengine waje kuwekeza. Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendelea kufanya mapitio ya sheria zetu kuondoa na kurekebisha sheria zote ambazo zimekuwa zikiwakwaza wawekezaji kuwekeza hapa nchini”.

Mheshimiwa Majaliwa alisema kukamilika kwa mradi huo soko la mifugo ikiwemo mbuzi ng’ombe na kondoo litakuwa na uhakika hivyo aliwataka Wananchi watumie fursa hiyo kuhakikisha wanafuga kwa wingi kwani soko la uwakika litakuwepo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema, “ Hivi tunavyoongea kila kitu kipo site, mitambo yote ya upozaji na mashine zote zipo, kazi ya ufungaji kama ulivyoona Mheshimiwa Waziri Mkuu inakamilika, ni matarajio kwamba mradi huu utakuwa umekamilika ndani ya miezi miwili ijayo, ambapo kazi ya ununuzi wa ng’ombe kwa ajili ya kunenepesha inaanza mwezi wa tisa”.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba akitoa maelezo ya mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru Hills, kwa Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martin Shigella.

Mradi ukikamilika utafanya mambo yafuatayo; uchinjaji wa ng’ombe 100 na mbuzi/kondoo 2,000 kwa siku, uzalishaji wa ajira za muda mrefu zisizopungua 350 na zaidi ya ajira 2,000 zitakazotokana na mnyororo wa thamani, Kuongeza kipato kwa wafugaji kwa kununua mifugo hapa hapa nchini, Kuongeza kipato kwa wakulima kwa kununua mazao ambayo yatatumika kwa kutengeneza chakula cha mifugo kwa ajili ya kunenepesha mifugo kabla ya kuichinja.

Pia mradi huo utaongeza mapato ya Taifa kupitia kodi mbalimbali kwa Serikali kuu na Halmashauri na  Kusaidia upatikanaji wa ngozi bora kwa viwanda vya kuchakata ngozi nchini kikiwemo kiwanda cha ngozi cha Kilimanjaro kinachomilikiwa na PSSSF na Jeshi la Magereza.

Watumishi wa PSSSF wakiwa pamoja na wafanyakazi wa mradi wa machinjio ya Nguru Hills, wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani) alipotembelea mradi huo.

Wafanyakazi wa mradi wa machinjio ya Nguru Hills, wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa(hayupo pichani) alipotembelea mradi huo.

Muonekano wa Majengo ya mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru, kulia ni sehemu ambayo mifugo itakuwa ikihifadhiwa na kushoto ni kiwanda cha kuchakata nyama.