*Lengo ni kuwa na uelewa pamoja

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeandaa mafunzo ya usimamizi wa Mikataba na Miradi kwa lengo la kuwajengea uwezo Watumishi ili Mfuko uweze kupata matarajio chanya katika miradi mbalimbali inayoendeshwa.

Watumishi wa Mfuko wanaohudhuria mafunzo ya usimamizi wa Miradi na Mikataba, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa PSSSF, Bw. Ernest Khisombi (aliyekaa katikati), Meneja wa kanda ya Ziwa Mashariki, Bw. Godfrey Mollel (aliyekaa kushoto) na Mkufunzi wa mafunzo hayo ni Mhandisi Paul Basondole.

Hayo yalisemwa Jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa PSSSF, Bw. Ernest Khisombi alipokuwa akifungua mafunzo kwa Watumishi wa Mfuko wanaohusika na usimamizi wa mikataba na miradi.

“Lengo ni kuweza kupata ufahamu na uelewa wa pamoja kati ya Watumishi wa Mfuko, katika kusimamia mikataba na miradi, ili Mfuko uweze kusimama vizuri ni lazima idara zote ziwe na uelewa wa pamoja,” alifafanua Bw. Khisombi.

Mkufunzi wa mafunzo ya usimamizi wa miradi na mafunzo, Mhandisi Paul Basondole akifundisha katika mafunzo hayo.

Bw. Khisombi alisema, Mfuko umeruhusu mafunzo hayo kufanyia ili kuwepo na utendaji wenye tija katika Mfuko baada ya mafunzo haya.

Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa PSSSF, Bw. Ernest Khisombi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa miradi na mikataba, Kushoto ni Meneja wa kanda ya Ziwa Mashariki, Bw. Godfrey Mollel.

Akizungumza awali, Meneja wa kanda ya Ziwa Mashariki, Bw. Godfrey Mollel aliwakaribisha washiriki wa mafunzo hayo jijini Mwanza na kusema, “Naamini baada ya mafunzo mtakuwa bora zaidi kwa maslahi mapana ya Mfuko”.

Mafunzo hayo yameanza Novemba 22, 2021 yataendelea hadi Disemba 3, 2021 ambapo Watumishi watahudhuria katika makundi mawili. Mkufunzi wa mafunzo hayo ni Mhandisi Paul F. Basondole, Mhandisi mwelekezi katika usimamizi wa miradi na mikataba.

Akizungumzia mafunzo hayo mmoja wa washiriki, Mhandisi Marco Kapinga, Meneja Miradi wa PSSSF, alisema, “Nategemea kutekeleza miradi kwa kufuata sheria za nchi, kusimamia miradi kwa weledi hususani katika kuzingatia matakwa ya mikataba na kuongeza uwezo wa wataalam wa ndani katika suala la uandaaji wa mkataba”.

Naye Nadya Khatibu, Ofisa Mkuu wa uwekezaji alisema baada ya mafunzo anatarajia kuongeza ufahamau, uelewa, udhibiti na usimamizi wa mikataba na miradi ya Mfuko.

Gloria Nguve, kutoka kurugenzi ya Ununuzi na Ugavi alisema, “ Kama kurugenzi tumefarijika kwa akuwepo kwa mafunzo haya, tunaamini kutokea sasa tunakwenda kusimimia vyema miradi na mikataba yote ya Mfuko kwa weledi”.

MATUKIO KATIKA PICHA: