*Wataka Mradi ukamilike vyema na kwa wakati

* Waongezewa ujuzi wa kudhibiti manunuzi

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Bodi ya zabuni ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imetembelea mradi wa ukarabati wa jengo la PSSSF Quality Plaza lililopo jijini Dar es Salaam na kuridhishwa na kazi zinazoendelea.

Mwenyekiti wa Bodi ya zabuni ya PSSSF, Bw. Gilbert Chawe (wa pili kutoka kushoto) akisisitiza jambo wakati yeye pamoja na wajumbe wengine walipotembelea mradi wa PSSSF Quality Plaza.

Ziara hiyo iliyofanyika mwanzoni mwa wiki kwa lengo la Bodi kukagua maendeleo ya mradi  wa maboresho katika jengo  hilo.  Kukamilika kwa matengenezo hayo kutaboresha jengo hilo na kutoa fursa kwa watu kuweza kupanga na kuendesha shughuli mbalimbali. Mradi huo unahusisha maboresho mbalimbali  ikiwemo mfumo wa umeme katika jengo hilo.

“Lengo la ziara hii, ni kujionea mambo tunayopitisha yanavyotekelezwa, hakika kuna mabadiliko ukilinganisha na mara ya mwisho tulipotembelea. Hata hivyo naomba kila kitu kifanyike kama kinavyoelekezwa kwenye mikataba na wote mnaohusika hakiksheni kazi inakamilika vyema  kwa kuzingatia ubora na kwa wakati” alifafanua Mwenyekiti wa bodi hiyo.

Kutoka Mwanza, inaripotiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya zabuni ya PSSSF, Bw. Gilbert Chawe amewashauri wajumbe wa bodi hiyo ambao walikuwa mafunzoni jijini Mwanza kutumia elimu waliyopatiwa kuhakikisha Mfuko unafanya manunuzi yenye tija.

Bw. Chawe alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akifunga mafunzo ya Upangaji na Usimamizi wa miradi iliyoandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Mfuko na kufanyika jijini Mwanza kuanzia Februari 23 hadi 25, 2022.

Wajumbe wa Bodi ya zabuni ya PSSSF wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Kurugenzi ya Manunuzi ya Mfuko na Mkufunzi wa mafunzo hayo baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo.

“Kutokana na mafunzo tusaidie taasisi  kufanya manunuzi yenye tija kwa mfuko, pia tuhakikishe mambo tunayopitisha kama bodi ya zabuni yawe sahihi, yanayozingatia sheria na maslahi ya taifa na Mfuko” alifafanua Mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya zabuni ya Mfuko Bw. Gilbert Chawe,akimkabidhi cha ushiriki cheti Bw. Fortunatus Magambo baada ya kumakizika kwa mafunzo ya wajumbe wa Bodi ya Zabuni. Wengine ni Bw. Ernest Khisombi (kushoto) na Mhandisi Paul Basondole (wa tatu kutoka kushoto) ambaye alikuwa Mkufunzi.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yaliwajumuisha wajumbe wote akiwemo Mwenyekiti Bw. Chawe, wajumbe wengine ni Bw. Paul Kijazi, Bw.Fortunatus Magambo, Bi. Beatrice Lupi, Bw. Victor Kikoti, Bi. Leila Maghimbi, Bw. Abdul Njaidi na Bw. Ernest Kishombi ambaye ni  katibu wa bodi hiyo. Pia katika mafunzo hayo Bi. Gloria Nguve na Bi. Malibiche kutoka kurugenzi ya manunuzi walihudhuria. Mkufunzi wa mafunzo hayo alikuwa Mhandisi Paul Basondole.

Imetumwa Machi 2, 2022