Na Mwandishi Wetu, Moshi

Katibu Mkuu katika ofisi ya Waziri Mkuu (Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Bw. Andrew Massawe ametoa maelekezo kwa Jeshi la Magereza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kuhakikisha mradi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Karanga unakamilika kwa wakati ili kianze uzalishaji.

Bw. Massawe alitoa maelekezo hayo alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi huo unaoendeshwa kwa ubia kati ya Jeshi la Magereza na PSSSF.

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Andrew Massawe (kushoto), akitoa maelekezo kwa wabia wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha karanga.

“Hakikisheni vifaa vya umeme vilivyoagizwa kwa kampuni za ndani vinapatikana, pia hakikisheni katika kiwanda kunakuwepo na ulinzi wa uhakika kwani kuna mashine za gharama kubwa” alisisitiza Bw. Massawe.

Kiwanda hicho kikikamilika kitaongeza uzalishaji wa viatu kutoka jozi 400 za sasa hadi jozi 4,000 kwa siku na kinatarajia kuzalisha ajira 7,000. kiwanda hicho kilichopo Karanga, Moshi mkoani Kilimanjaro ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA. Hosea Kashimba ambaye alisema, “tutahakikisha ujenzi haukwami, tutashirikiana vyema na wenzetu kwa lengo la kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA. Hosea Kashimba (wa pili kulia) akifafanua jambo kwa wabia wenzake wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha karanga.

Majengo ya Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga ambayo yamekamilika kwa asilimia 95.