*Rais Samia apongeza Wanawake kwa kudumisha amani, utulivu

*Wanawake PSSSF washiriki maadhimisho

Na Waandishi Wetu,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshiniwa Samia Suluhu Hassan ameitumia siku ya wanawake duniani kuwapongeza wanawake kote nchini kwa jinsi wanavyojitoa katika kujenga uchumi wa Tanzania.

Aliyasema hayo jana mjini Unguja katika viwanja vya Maisara katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wanawake duniani na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr. Hussein Ali Mwinyi.

“Katika siku hii ya Wanawake Duniani, nawapongeza wanawake wote kwa mchango wenu katika kujenga uchumi, kustawisha jamii na kudumisha Amani na utulivu” alisema Mheshimiwa Rais. Kaulimbiu ya siku hii muhimu ni “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu:Tujitokeze Kuhesabiwa”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali katika madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Kitaifa imefanyika katika Viwanja vya Maisara Zanzibar (picha kwa hisani ya Ikulu).

Katika hatua nyingine: Watumishi Wanawake wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wameshiriki maandamano yaliyofanyika nchini kote kupitia uratibu uliofanywa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa. Wakitoa maoni yao kuhusu umuhimu wa siku hii, Afisa Mwandamizi Huduma kwa Wateja, Bi. Asha Baruti amesema; “Siku nzuri, wameandaa vizuri, ushirikiano mzuri, tunaushukuru Mfuko kwa kutujali”.

Akielezea umuhimu wa siku hii, Bi. Asha alisisitiza kwamba wanawake wana nguvu kubwa ukiwapa fursa wana uwezo wa kufanya mambo makubwa kwa kuwa wanawake ni watimiza majukumu na hivyo wanapaswa kuaminiwa.

Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF, waliokaa kutoka kushoto ni CPA. Stella Katende, Bi. Suzan Kabogo na Bi. Mazoea Mwera, wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mfuko. Wajumbe hao walipiga picha hiyo ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Bodi ya PSSSF inaendelea na mafunzo jijini Arusha.

Naye, Bi. Bertha Mapunda, Afisa Kumbukumbu Ofisi ya PSSSF Makao Makuu Ndogo, Dar Es Salaam, aliushukuru Uongozi wa PSSSF kwa kuonesha upendo kwenye siku hii na kuelezea furaha yake kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, ambayo yamekuwa bora zaidi.

Aidha aliwaasa wanawake kuendelea kushirikiana na kusaidiana ili kuweza kufikia malengo.  “Wanawake tubebane, mshike mkono mwenzako, tupendane, ukipanda panda na mwenzio”, alisisitiza.

Watumishi wa PSSSF ofisi ya mkoa wa Mwanza, wakiwa katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Nyamagana.

Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila tarehe 8 ya mwezi Machi kila mwaka.

Imetumwa, Machi 8, 2022