*Kwa kuanzia wasaini makubaliano ya trilioni 2.17

*Katibu Mkuu: Deni linalipwa kwa utaratibu wa hati fungani maalum

*PSSSF: Tutaendelea kutoa huduma bora kwa Wastaafu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wizara ya Fedha na Mipango imetoa pongezi kwa serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo ambayo yamepelekea kuhitimisha suala la muda mrefu kwa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Kauli hiyo ilitolewa na katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba Desemba 22, 2021 jijini Dodoma katika sherehe ya utiaji sani makubaliano ya ulipaji wa shilingi trillioni 2.17 kwa PSSSF.

Bw. Emmanuel Tutuba alisema, “Sisi kama Wizara tumekuwa na majadiliano mara kadhaa na uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na sasa PSSSF juu ya kulishughulikia deni hili, baada ya kufanya uchambuzi wa kina juu ya suala hilo na kwa maslahi mapana ya wanachama wa Mfuko, Serikali imeamua kulipa deni hilo kwa kuanzia na shilingi trilioni 2.17, na deni hilo litalipwa kwa utaratibu wa hati fungani zisizo taslimu”.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba (wa pili kutoka kulia waliokaa) na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kushoto waliokaa) wakisaini hati za makubaliano ya ulipaji wa shilingi trilioni 2.17, anayeshuhudia kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu, Prof. jamal Katundu.

Bw. Tutuba alisema katika hotuba ya Bajeti ya serikali ya mwaka 2021/2022 Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba alibainisha umuhimu wa wastaafu wa taifa letu ambao wamelitumikia taifa kwa uzalendo na uadilifu wa hali ya juu kupata stahiki zao kwa wakati. Katika kufanikisha hilo Waziri wa fedha aliahidi kuendelea kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutoa hatifungani maalum.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Jamal Katundu alitoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulisimamia vyema na ukaribu suala la deni la PSSSF, ambalo linatoa faraja kwa wanachama wa PSSSF wakiwemo Wastaafu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kushoto) wakionesha hati za makubaliano ya ulipaji wa shilingi trilioni 2.17, anayeshuhudia kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu, Prof. jamal Katundu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema, “Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, tunatoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake kwa kuweza kushughulikia suala hili ambalo limekuwepo kwa muda mrefu na kupatiwa ufumbuzi chini ya utawala wake. Kwa upande wetu tunaahidi kuendelea kufanyakazi kwa weledi katika kutoa huduma bora kwa wanachama wetu”.

CPA.Kashimba alisema, makubaliano hayo ya 2.17 trilioni ambayo ni sehemu ya deni la Pre 1999 la 4.6 yatasaidia Mfuko kupata mapato yanayotokana na hati fungani hizo takribani shilingi bilioni 120 kwa mwaka ambazo zitauwezesha Mfuko kupata unafuu wa deni la pre 1999 na pia kuuwezesha kutimiza jukumu lake la msingi la kulipa mafao.

Katika sherehe hizo Serikali iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha Bw. Tutuba na kwa upande wa PSSSF iliwakilishwa na CPA. Kashimba. Pia ofisi ya Waziri Mkuu iliwakilishwa na Naibu Katibuy Mkuu, Prof. Jamal Katundu.

Maafisa wa PSSSF, wakishuhudia utiaji saini makubaliano ya ulipaji wa shilingi trilioni 2.17, kati ya Serikali na PSSSF.

Maafisa wa Wizara ya Fedha, wakishuhudia utiaji saini makubaliano ya ulipaji wa shilingi trilioni 2.17, kati ya Serikali na PSSSF.