*Apongeza PSSSF na Magereza kwa uwekezaji wenye tija

*Ataka kiwanda kikamilike kama ilivyokusudiwa

*Mhagama: Tumetekeleza maelekezo ya kuwekeza kwenye viwanda

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuanza utendaji kazi vyema kwa kuwekeza kwenye viwanda ambavyo vina tija kwa taifa.

Dkt. Magufuli alisema hayo mjini Moshi wakati akizindua kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya PSSSF na Jeshi la Magereza.

“Nawapongeza sana PSSSF kwa kuanza vyema, zamani Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikwa ikiwekeza katika majengo ambayo yalikuwa na faida ndogo sana, lakini baada ya kuanza kuwekeza kwenye viwanda kama hiki cha Kilimanjaro, uwekezaji huu unatoa fursa kwa wengi ikiwemo ajira kwa watanzania” alisema

Dkt.John Joseph Magufuli akiangalia mtambo wa kuzalishia viatu katika sherehe za ufunguzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro.

Aliongeza pia kwa kutoa pongezi kwa Jeshi la Magereza kwa kukubaki kuingia ubia na PSSSF, kiwanda hiki kinatimiza ndoto ya miaka mingi ya Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarge Nyerere ambaye katika uongozi wake kiwanda cha kwanza cha ngozi kilijengwa mjini Moshi mwaka 1978.

“Najua ngozi nyingi haitoki hapa, kiwanda hiki kimejengwa hapa Kilimanjaro ili kukamilisha malengo ya Baba wa Taifa, pia nilikubali kiwanda hiki kijengwe kwa mapenzi ya serikali kwa watu wa mkoa wa Kilimajaro,” alifafanua

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisisitiza watanzania kupenda vitu vinavyozalishwa nyumbani ikiwemo bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kiwanda cha Kilimanjaro.

“Kuazishwa kwa kiwanda hiki, nina imani kwamba baada ya mwaka mmoja, kila mmoja wetu atakuwa amevaa viatu vinavyotengenezwa na kiwanda chetu cha Kilimanjaro,” alisema

Katika kuhakikisha kiwanda hicho kinakamilika kwa wakati, Mhe. Rais alisema, “Natoa wito kiwanda hiki kwa ujumla wake kikamilike kwa wakati na bidhaa za kiwanda ziwe bora ili ziweze kupata soko”

Akizungumza awali Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alisema Ujenzi wa mradi huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa tarehe 9 Mei, 2016 wakati wa ufunguzi wa majengo ya vitega uchumi vya PSSSF na NSSF jijini Arusha ambapo alielekeza Mifuko kuwekeza zaidi katika viwanda badala ya majengo ili kukuza ajira na kuendeleza uchumi.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Mjini Moshi katika ufunguzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro.

Akitoa taarifa ya uendeshaji wa kampuni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea kashimba alisema kuwa uwekezaji katika kiwanda hicho  Mfuko wa PSSSF unamiliki asilimia 86 na Jeshi la Magereza asilimia 14. Jeshi la Magereza likiwa limechangia eneo la kiwanda lenye hekari 25 (mita za mraba 100,000) pamoja na kiwanda cha zamani na Mfuko wa PSSSF unachangia gharama za ujenzi wa majengo, ununuzi wa mashine na mitambo pamoja na gharama za uendeshaji.

“Mpaka kukamilika kwake mradi huu unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 136 ikijumuisha gharama za ardhi, ujenzi wa majengo, mashine na mitambo, ushuru wa forodha na gharama za uendeshaji na mtaji wa kuendesha kiwanda  alifafanua CPA. Kashimba” alifafanua

Aliongeza kuwa, Kiwanda kitakapo kamilika kinatarajiwa kuzalisha jozi za viatu milioni 1.2 kwa mwaka, soli za viatu jozi laki 9 mpaka milioni 2.1 kwa mwaka, bidhaa mbalimbali. Aidha, kiwanda cha kuchakata ngozi (tannery) kitakuwa na uwezo wa kuchakata futi za mraba (Sq.ft.) milioni 13 kwa mwaka, ambazo asilimia 60 zitatumika kiwandani na asilimia 40 kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi

Akizungumzia faida ya kiwanda hicho, CPA. Kashima alisema, Mradi huu utakuwa na faida mbalimbali kama ifuatavyo;Kuwa kitega uchumi mahususi kwa ajili ya kulinda thamani ya uwekezaji uliofanywa na Mfuko PSSSF na Jeshi la Magereza; Kupatikana kwa soko la uhakika la ngozi ghafi kutoka kwa wafugaji, Kuongezeka thamani ya ngozi inayozalishwa hapa nchini kutokana na mpango wa mafunzo maalumu kwa wafugaji na ajira za moja kwa moja 3000 na zaidi ya ajira 7000 zisizo za moja kwa moja katika mnyororo wa thamani na huduma.

Faida nyingine ni; Kuongeza mapato kwa Taifa kupitia kodi mbalimbali, Mradi utakuwa na manufaa makubwa kwa mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa jirani kwa kuboresha mfumo wa maisha na kuongeza kipato kwa wakazi, majengo na miundombinu na Kuokoa fedha za kigeni kwa kupunguza uingizaji wa bidhaa za ngozi nchini na kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa za ngozi nje ya nchi

Uzinduzi wa kiwanda hicho ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi wa mji wa Moshi. Pamoja na wananchi hao pia viongozi mbalimbali wakiwemo, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa dini na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

Mei mwaka 2017, Mfuko uliokuwa wa PPF (sasa shughuli zake zikitekelezwa na PSSSF) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza walianzisha Kampuni ya ubia iliyojulikana kwa jina la Karanga Leather Industries Co. Ltd ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina la “Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd”. Kampuni hii inamilikiwa na Mfuko wa PSSSF kwa asilimia 86 na Jeshi la Magereza kwa asilimia 14.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akifungua jiwe la msingi katika ufunguzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro.