Na Mwandishi Wetu, Singida

 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umefanya mafunzo kuhusu Ukimwi na Magonjwa yasiyoambukiza, mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kilichopo mkoani Singida kuanzia Aprili 20 hadi 22.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bi. Esther Mwamyalla alimshukuru Mkurugenzi Mkuu pamoja na Menejimenti kwa kuratibu mafunzo hayo ili kuwawezesha Watumishi kupata uelewa juu ya UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa ambayo mara nyingi huwapata watumishi walipo makazini pamoja na jamii zinazowazungunguka.

Magonjwa hayo yasiyoambukizwa ni pamoja na Kisukari, Shinikizo la Damu, Kiharusi, Kansa, Pumu, Figo na mengineyo ambayo huweza kumpata mtu yoyote pasipo kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenzake. Magonjwa yasiyoambukizwa hupatikana aidha kwa mabadiliko ya mwili kutokana na umri, jinsia, kazi na mazingira au kwa mtu husika kutofuata taratibu mbalimbali za afya bora.

Meneja wa Utawala Bi. Esther Mwamyalla (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa PSSSF, pamoja na Mkufunzi wa Mafunzo hayo Dkt. Jaffari Ndege (wa kwanza kulia).

Hata hivyo Bi. Esther alisisitiza watumishi kujikinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI na kuchukua tahadhari ili kuweza kuzuia maambukizi mapya ambayo huambukizwa kwa njia mbalimbali.“Watumishi waliohudhuria mafunzo haya kwa kweli wameonesha umakini wa hali ya juu kwa kile walichokipata kutoka wakufunzi wa mafunzo hayo na nina imani watafikisha elimu hii kwa Watumishi”, alisema Bi. Esther Mwamyalla.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Bi. Grace Fihavango, alimshukuru Mkurugenzi Mkuu pamoja na Menejimenti kwa kupata mafunzo hayo kwa kuwa ameweza kujua mambo mengi yanayohusu UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa na atahakikisha elimu hiyo kwa watumishi wengine.

Dkt. Jaffari Ndege akifundisha kuhusu UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa.

Watumishi wa PSSSF wakiwa katika mafunzo ya Ukimwi na magonjwa yasiyoambukizwa

“Imekuwa fursa nzuri kwetu maana kuna vitu nilikua sijui vizuri na nilikua nakisia kisia kuhusu UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa, ila kwa sasa nimeweza kuelewa vizuri na ninaahidi kuwa balozi mzuri kwa wenzangu pamoja na familia yangu kwa ujumla, na pia nimeweza kupata fursa ya kukutana na wenzangu ambao hatujawahi kuonana” alisema Bw. Kiwamba Njau wa Ofisi ya PSSSF Geita.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kilichopo mkoani Singida, yakifundishwa na madaktari kutoa Hospitali ya mkoa wa Singida.