*Msigwa: Semina imetujengea uelewa
*PSSSF: Tunaendele kutatua kero za Wanachama

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Mkurugenzi wa idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amesema taasisi zikifanyakazi zake vyema zinawapunguzia kazi ya kutoa ufanunuzi mara kwa mara juu ya taasisi husika.
Msemaji Mkuu wa Serikali alisema hayo Oktoba 15, 2021 jijini Mwanza katika semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) maalum kwa ajili ya Watumishi wa ofisi ya Msemaji Mkuu wa serikali kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya PSSSF.
“Mkurugenzi tunashukuru kwa semina hii, kwani ni muhimu sana katika utendaji kazi wetu wa kuisemea serikali…pia imetusaidia kujua masuala yetu ya kiutumishi” alifafanua Bw. Msigwa

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (Kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati wa kikao kazi hicho.

Akizungumia utendaji kazi wa PSSSF, Msemaji Mkuu wa Serikali alisema, “Kwa sasa naona mnajitahidi sana kujibu hoja mbalimbali, hakika mnafanyakazi nzuri, hongereni sana na endeleeni hiyohiyo”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba akizungumzia semina hiyo alisema, “Sekta yetu ni nyeti, na huu ndio msingi wa kuwaomba kuwa na kikao na ofisi ya Msemaji wa Serikali”.
Akizungumzia malalamiko mbalimbali kutoka kwa Wanachama, CPA. Kashimba alisema, malalamiko yapo na tumejipangia mpaka kufikia mwisho wa Disemba mwaka huu malalamiko yote yawe yametatuliwa.
“Nashukuru kwa semina hii, naamini imekuwa ya muhimu kwetu wote, tuzidi kuona namna ya kuendeleza ushirikiano huu” alisisitiza CPA. Kashimba.
Semina hiyo iliyofanyika jijini Mwanza, imekutanisha Watumishi kutoka ofisi ya msemaji mkuu wa serikali, Watumishi wa PSSSF kutoka Makao Makuu Dodoma na ofisi ya PSSSF mkoa wa Mwanza.

Happiness Manyeye wa PSSSF Mwanza, akitoa mada wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika.

Baadhi ya watumishi wa Idara ya Habari-MAELEZO wakifuatilia jambo wakati wa kikao kazi hicho.