• CPA Hosea Kashimba amshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi na hivyo kufungua fursa za uwekezaji na biashara
  • CPA Innocent Rwetabura afurahia mazingira bora ya Makao Makuu mapya yatakayochagiza umoja na ubunifu miongoni mwa wafanyakazi
  • Ni jengo refu zaidi nchini na miongoni mwa majengo marefu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba leo ametia saini mkataba wa upangishaji wa makazi ya ofisi na Kampuni ya MIC Tanzania PLC inayomiliki kampuni ya TIGO na Zantel, katika jengo jipya la PSSSF Commercial Complex lililoko Sam Nujoma Jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo fupi ilihudhuriwa na viongozi kutoka PSSSF, MIC na GIMCOAFRICA ambao ndio kampuni inayosimamia jengo hilo.  Akiwasilisha hotuba yake, CPA Kashimba alisema utiaji saini wa mkataba huu ni mwanzo wa mahusiano ya kibiashara kati ya taasisi hizi mbili na kwamba amefarijika na uamuzi wa MIC kuhamishia Makao Makuu yake hapo.

“Ni fahari kubwa kwa taasisi zetu kukutana pamoja hapa siku ya leo kwa ajili ya hafla ya utiaji saini wa mkataba wa upangishaji ambao unaashiria ukurasa mpya wa mahusiano kati ya PSSSF na TIGO.  Ninasema karibuni sana PSSSF, hapa ni nyumbani kwenu” alisema CPA Kashimba

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba (kulia) akitia saini na Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Tigo CPA. Innocent Rwetabura (kushoto), mkataba wa upangishaji wa makazi ya ofisi na Kampuni ya MIC Tanzania PLC inayomiliki kampuni ya TIGO na Zantel, katika jengo jipya la PSSSF Commercial Complex lililoko Sam Nujoma Jijini Dar es Salaam.

Akishukuru kwa ukaribisho huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIGO CPA Innocent Rwetabura alisema; “lengo ni kuongeza ufanisi na kuziweka pamoja Tigo na Zantel ili kujenga mazingira bora yatakayochagiza umoja na ubunifu miongoni mwa wafanyakazi wetu ili kwa pamoja tuweze kutengeneza bidhaa na kutoa huduma za hali ya juu kwa wateja wetu zaidi ya milioni 14 kote nchini”.

Akiongelea fursa zinazoweza kupatikana kutokana na uwepo wa TIGO kwenye jengo la PSSSF Commercial Complex, CPA Kashimba pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada zinazofanyika na kusema; “Nipende pia kumshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anayofanya ya kufungua nchi pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kibiashara. Jitihada hizo pamoja na mambo mengine ndio matokeo tunayoyaona ya kuongezeka kwa wapangaji katika majengo yetu”.

Akihitimisha hotuba yake CPA Kashimba aliwashukuru TIGO kwa uamuzi sahihi wa kuhamishia ofisi zao za Makao Makuu kwenye kitegauchumi hiki kipya na pia aliwashukuru GIMCOAFRICA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia na kupangisha jengo.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba (kulia) wakibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Tigo CPA. Innocent Rwetabura baada ya kutia saini ya upangishaji wa makazi ya ofisi na Kampuni ya MIC Tanzania PLC inayomiliki kampuni ya TIGO na Zantel, katika jengo jipya la PSSSF Commercial Complex lililoko Sam Nujoma Jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo fupi ya utiaji saini ilihudhuriwa na watendaji wakuu kutoka taasisi zote mbili za PSSSF na MIC – TIGO pamoja na GIMCOAFRICA.

Jengo la PSSSF Commercial Complex ni jengo kubwa zaidi la kibiashara hapa nchini kwa sasa.Mradi wa ujenzi ulianzishwa na uliokuwa Mfuko wa PPF.  Jengo la PSSSF Commercial Complex lina eneo la kupangisha lenye ukubwa wa mita za mraba 74,000 zinazojumuisha Jengo la “executive” lenye ghorofa 14 mahsusi kwa ajili ya maofisi,  ukumbi wa shughuli za kibenki na ukumbi wa mikutano.   Vilevile Jengo la biashara lenye ghorofa 35; Jengo lenye ghorofa 3 la kumbi za mikutano zenye kumbi zenye uwezo wa kuchukua watu 15 hadi 900 kwa wakati mmoja pamoja na vyumba vya kupumzikia wageni mashuhuri (VIP); na Jengo la maegesho ya magari lenye ghorofa 6 lenye uwezo wa kuegesha magari zaidi ya 830 kwa wakati mmoja pamoja na eneo la mgahawa, bwawa la kuogelea, mazoezi na burudani lililoko ghorofa ya 5.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA Hosea Kashimba (wa pili kutoka kulia waliokaa)  na Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Tigo CPA. Innocent Rwetabura (wa tatu kutoka kushoto waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa PSSSF  na Tigo.