*Yaongoza upande wa Taasisi za Pensheni na Bima za Afya

*Ushindi unaashiria ueledi,nidhamu na umahiri wa Watumishi

*Dhamira kuu ni utunzaji makini wa michango ya wanachama na Rasilimali za Mfuko.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF umetunukiwa tuzo ya umahiri ya uandaaji wa taarifa za fedha kwa mwaka 2020 zilizotolewa jana na NBAA katika hafla maalum iliyofanyika  katika kituo cha Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kilichopo Bunju, Jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo Imekabidhiwa kwa PSSSF na Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA.Leonard Mkude.

Akipokea tuzo hiyo Mkurugenzi wa Fedha Bibi Beatrice Musa-Lupi amewapongeza watumishi kwa kufanya kazi kwa ueledi na kuzingatia viwango vilivyowekwa. “Ushindi huu unaonesha kuna weledi kwa watumishi wetu kwasababu bila ya watumishi wanaofanya hizi kazi kila siku tusingeweza kufikia hapa”; alisisitiza Bibi Beatrice Musa-Lupi.

Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (kulia) akipokea tuzo hiyo kutoka kwa mgeni rasmi, Mhasibu Mkuu wa Serikali Bw. Leonard Mkude.

Jumla ya Taasisi za Umma na Binafsi 71 zilishiriki katika tathmini hizi. Akihutubia katika hafla hii Mgeni Rasmi alisema wawekezaji, walipakodi, wadau mbalimbali na wananchi wanategemea taarifa za mahesabu ili kufanya maamuzi mbalimbali  hivyo basi Taasisi zinapaswa kujikita kuandaa mahesabu kitaalam na kwa kufuata viwango na vigezo vilivyowekwa.

Aidha Mgeni Rasmi alisisitiza taasisi kuendana na kasi ya maendeleo ya kidijitali na kuiendesha kada ya Uhasibu kuendana na mapinduzi ya kidijitali.

Hafla hiyo ya kugawa tuzo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Watumishi wa Mfuko kutoka Kurugenzi ya Fedha, Kurugenzi ya Ukaguzi na Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha Bibi Beatrice Musa-Lupi.

Washindi wa Kwanza wa tuzo zilizotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu.

Akiongelea kuhusu umuhimu wa uandaaji na uwasilishaji bora wa taarifa za mahesabu, Bibi Lupi aliongeza; “Ushindi huu ni hakikisho kwa wanachama kuwa mali zao ziko salama na kwamba zinalindwa kwa kufuata taratibu na Sheria za Nchi, Sheria za Kimataifa pia”.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya NBAA CPA Neema Msusa amezishukuru taasisi zote zilizoshiriki kwenye ushindani, kudhamini na kuhudhuria katika hafla zote zilizoandaliwa na NBAA.

Baadhi ya Taasisi zilizotunukiwa tuzo za NBAA, ni pamoja na CRDB, TRA, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya, NHIF, SANLAM, TASAC, Manispaa ya Ilala na

Tanesco.

Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Bi. Beatrice Musa-Lupi (katikati), akiwa na watumishi wa PSSSF katika picha ya pamoja.