*Lengo ni kupunguza gharamna za uendeshaji

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewakaribisha wabunifu nchini kutembelea viwanda ambavyo PSSSF imewekeza kwa ubia kwa lengo la kuona njia ya kusaidia viwanda hivyo kupata teknolojia itakayosaidia kuzalisha bidhaa kwa gharama nafuu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akimkabidhi Hati Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba kwa kutambua mchango wa Mfuko wa Mfuko wa PSSSF katika kufanikisha maonesho ya Mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu(MAKISATU) yaliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Mei 2021.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Hosea kashimba, pembeni mwa Maonesho ya Mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu (MAKISATU) yaliyomaliza jijini Dodoma na kufungwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu.

“PSSSF ipo kwenye ubia wa kuendesha viwanda kadhaa ikiwemo Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro, mradi wa machinjio na kuchakata nyama na kiwanda cha kusindika tangawizi, hivyo tunaamini wabunifu wetu wanaweza kubuni teknolojia kwa ajili ya viwanda hivyo ambazo zitapatikana kwa gharama nafuu na kupunguza gharama za uendeshaji” alishauri Bw. kashimba.

Mfuko umewekeza katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro kilichopo Moshi, mradi wa machinjio na kuchakata nyama wa Nguru Ranch uliopo Morogoro na kiwanda cha kuchakata tangawizi cha Same. Lengo la mfuko ni kusaidia wakulima wadogo na kuendeleza zao la tangawizi.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya Pamoja na wadau waliofanikisha maonesho hayo.