*Mlowe: Tutaendeleza utamaduni wa huduma bora kwa mteja

*Huduma iliyotukuka kwa wanachama ni haki ya kila mwanachama

Katika kusheherekea Wiki ya Huduma kwa Wateja, wanachama wa PSSSF mkoani Tanga wamepongeza huduma wanayopatiwa siku kwa siku kuwa ni ya haraka na yenye kuzingatia weledi.

Akiongea kwa niaba ya wastaafu waliokuja kupatiwa huduma katika Ofisi za PSSSF Tanga, mstaafu Mwl. Valen- tine Ngoiya Adriano alisema “huduma za ofisi ya PSSSF Tanga ni zenye kuzingatia weledi na uharaka ambayo inatusaida kupata majibu ya madai yetu kwa wakati” Akielezea ni nini anachotegemea kama mteja na mwanachama wa PSSSF, Mwl Valentino, alisema baada ya kutumikia Serikali kwa kipindi kirefu anategemea kupata huduma kama mteja anayethaminiwa kwa kujali utumishi uliotukuka ambao ameutumikia katika Taifa. Alitoa rai kwa uongozi wa Mfuko wa PSSSF kutoa elimu juu ya mafao ili wastaafu waweze kuwa na matumizi sahihi ya kiinua mgongo ambacho wamepata katika uzee wao. “Wastaafu wengi hupoteza pesa ambazo wamepata kama kiinua mgongo kwa sababu ya kuingia katika biashara ambazo kimsingi haziendani na umri wao na hivyo kupoteza pesa na matokea yake kuishi maisha ya uzee ambayo hayana staha”.

Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe akiongea na wanachama wa PSSSF Mkoani Tanga katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, 2021.

Akiongea na wanachama waliokuja kupata huduma katika ofisi za PSSSF Tanga, Meneja wa Huduma kwa Wateja, Bi. Laila Maghimbi, alisema katika Wiki ya Huduma kwa Wateja PSSSF inasheherekea kazi kubwa inayofanywa na watumishi wa PSSSF ya kuangalia na kulinda maslahi ya wanachama. “Ni muda pia tunapata kama watumishi wa Mfuko kuangalia kwa undani namna ambavyo tunahudumia wanachama wetu, kuboresha huduma zetu na kuona ni namna gani tunaweza kuboresha kwa kutoa huduma bora zaidi.”

Akiongea na wanachama kwa nyakati tofauti, Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe, alisema muda huu unatupatia nafasi nzuri ya kujiuliza mteja wetu anataka nini? “Hii inatusaidia kuendeleza utamaduni wa huduma kwa mteja na matokeo yake ni kwamba utamaduni huu polepole unaingia katika utamaduni wa utendaji kazi wa watumishi wa Mfuko. Alimalizia kwa kusema huduma iliyotukuka kwa wanachama wetu ni haki ya kila mwanachama. “Bila wanachama hakuna PSSSF, hivyo basi kila mmoja wetu ana wajibu wa kutoa huduma bora kwa maslahi mapana ya Mfuko wetu na wanachama. Wiki ya Huduma kwa Wateja ni siku inayosheherekewa na mashirika na taasisi kimataifa popote duniani inayosisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa huduma kwa wateja kwa kukuza uimara wa taasisi.

MATUKIO KATIKA PICHA:

Kaimu Meneja wa PSSSF Mkoa wa Tanga, Bw. Nyemo Chomola akiongea na wanachama wa PSSSF Mkoani Tanga katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, 2021.

Sehemu ya wanachama wa PSSSF waliokuja kupata huduma katika Ofisi za PSSSF Tanga.

Meneja wa Huduma kwa Wateja wa PSSSF, Bi. Laila Maghimbi, akitoa huduma kwa mwanachama katika Ofisi za PSSSF Tanga.

Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. James Mlowe, akimhudumia mwanachama wa PSSSF Mkoani Tanga.