*Semina itaiongezea uelewa ofisi ya Msemaji

*PSSSF kuendelea kukutana na wadau

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

OFISI ya Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali imetoa pongezi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kusogeza huduma zake karibu na Wanachama wake nchi nzima ikiwemo Pemba, Ifakara, Korogwe na Kahama.

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Rodney Thadeus katika semina juu ya huduma, utendaji na mafao yanayotolewa na PSSSF kwa watumishi wa ofisi ya Msemaji Mkuu wa serikali yaliyofanyika mkoani Morogoro Januari 29, 2022.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Bw. Rodney Thadeus akizungumza wakati wa kikao kazi hicho.

“Kwa kweli nimefarijika sana kusikia kuwa huduma zenu zimefika hadi Ifakara, hii ndio inayotakiwa, kuhakikisha Wanachama wenu wanapata huduma popote walipo, hongereni sana, endeleeni kuwasogezea huduma Wanachama wenu” alishauri Bw. Thadeus ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi-Huduma za Habari.

Mkurugenzi huyo alitoa pongezi kwa PSSSF kwa kuwasogezea huduma wanachama wake kwa kutumia mitandao ya kijamii na simu za mikononi, alisema hatua hiyo ni kubwa na inawawezesha wanachama kupata huduma wakati wowote na popote walipo.

Bw. Thadeus alisema PSSSF ni Mfuko muhimu sana kwa maisha ya Watanzania haswa Wastaafu ambao wamelitumikia taifa kwa uzalendo mkubwa, hivyo aliwataka watumishi wa PSSSF kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama hao.

Akizungumzia mafunzo hayo Bw. Thadeus alisema, “Idara ikiujua Mfuko (PSSSF) vyema itasaidia sana Watumishi wa ofisi ya Msemaji kutoa taarifa sahihi za PSSSF pale wanapohitajika kufanya hivyo”. Pia Mkurugenzi huyo alishukuru kwa uwepo wa ushirikiano chanya kati ya PSSSF na ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Mbaruku Magawa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji akizungumza wakati wa kikao kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw.Mbaruku Magawa alimshukuru Msemaji Mkuu wa serikali pamoja na watumishi katika ofisi hiyo kwa kuweze kutenga muda kwa ajili ya semina hiyo, alisema pamoja na kazi nyingi katika ofisi hiyo lakini waliweze kujipanga na huhudhuria semina hiyo ambayo ilikuwa ni mwendelezo wa semina kama iliyofanyika jijini Mwanza Oktoba 15, 2021.

“Tunaamini iwapo ofisi ya Msemaji Mkuu mkituelewa vyema itakuwa rahisi kwenu kufikisha taarifa kwa wananchi popote mnapokuwa mnatoa taarifa mbalimbali za serikali…katika semina ya leo kutakuwa na mada za huduma na mafao ya PSSSF, mada ya uwekezaji, baada ya hapo kutakuwa na muda wa maswali na majadiliano” alifafanua Bw. Magawa ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko.

PSSSF imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu juu ya utendaji, huduma na mafao yanayotolewa na PSSSF, Januari 15, 2022 ilikutana na Jukwaa la Wahariri kwa lengo kama hili na ina ratiba ya kukutana na wadau wengine. PSSSF inaamini kuwa wadau wakiujua vyema Mfuko utarahisisha utendaji wake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Mbaruku Magawa (Wa pili kutoka kulia waliokaa) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO ,Bw. Rodney Thadeus (wa tatu kutoka kulia waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa idara ya Habari MAELEZO na Watumishi wa PSSSF.