*Ni kwa kuanzishwa kwa kiwanda cha bidhaa za ngozi

*Afungua kikao cha wadau wa ngozi jijini Mwanza

*Awataka wadau kuhakikisha kiwanda kinaenda vyema

Na Waandishi Wetu, Mwanza

Serikali imepongeza ubia kati ya Jeshi la Magereza na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuwa ni kiashiria cha wazi cha namna Taasisi za umma zilivyopokea na kuamua kutekeleza kwa vitendo Sera na maagizo ya Serikali ya kuwa wadau muhimu katika kujenga uendelevu wa Uchumi kupitia Viwanda.

Hayo yamesemwa na Waziri wa nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB), wakati akifungua kongamano la wadau wa sekta ya ngozi lilifanyika jijini Mwanza, Septemba 29, 2020.

“Tarehe 13 Agosti, 2020 nilipofanya ziara yangu mkoani Kilimanjaro nikiambatana na Katibu Mkuu wangu Bw. Andrew Massawe, kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa Kiwanda hiki (Kilimanjaro International Leather Industry) na niliagiza kufanyika kwa tathmini ya maeneo muhimu ambayo yanatakiwa kupata ufumbuzi wa haraka kabla kiwanda hakijaanza kufanya kazi. Ninafuraha kuona leo kupitia kongamano hili la Wadau wa Sekta ya Ngozi na mazao yake mnakwenda kujadiliana na kuyapatia muafaka masuala muhimu ya uendeshaji na uzalishaji wa kiwanda kama nilivyoagiza” alifafanua Mhe Mhagama.

Mhe. Mhagama amesema kupitia kongamano hilo anatarajia masuala yafuatayo kupatiwa ufumbuzi; Upatikanaji wa ngozi ghafi zenye ubora stahiki, Mpango wa uendelevu wa upatikanaji wa malighafi pamoja, Uendelevu wa kiwanda na uzalishaji na Upatikanaji wa masoko ya bidhaa za ngozi.

Mhe. Waziri alisema amefurahi kwamba wataalam kutoka taasisi zetu za ndani kuanzia wizara husika ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Taasisi ya Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), na Chama cha Wadau wa Ngozi Tanzania (LAT) wameshiriki kongamano hili. Hivyo anaamini kongamano litakwenda vizuri na litakua lenye mafanikio makubwa.

Aidha Mhe. Mhagama amempongeza, Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya Tano kwa kutupatia uongozi bora wenye maono makubwa ya kupaisha uchumi wa Tanzania kupitia Viwanda, Mhe Waziri aliendelea kusema, “Ni katika msingi huo sisi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu tulielekeza na kusimamia Mfuko wa PSSSF na kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Magereza waweze kuanzisha kiwanda cha bidhaa za ngozi. Hivyo; nawapongeza sana”.

Makatibu Wakuu waliohudhuria kikao hicho wote kwa wameahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kiwanda hicho kinafanyakazi vizuri, kinapata malighafi, kinapata masoko na utaalam wa kukiendesha.

Makatibu Wakuu waliohudhuria ni pamoja na Bw. Christopher Kadio, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani, Profesa Elisante Ole Gabriel katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Riziki Shemdoe, katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Bishara na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya kazi. Pia wadau mbalimbali katika sekta ya ngozi walihudhuria.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Hosea kashimba alisema, “Katika kuunga Mkono Jitihada za Rais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk John Joseph Pombe Magufuli za kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda, Mfuko Wa PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza tumewekeza katika Mradi wa ubia wa ujenzi wa Kiwanda cha ngozi na bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro”.

Bw.Kashimba alisema mradi huo unamilikiwa na PSSSF kwa asilimia 86 na Jeshi la Magereza kwa asilimia 14. Ubia huo umelenga kuboresha kiwanda cha bidhaa za ngozi kilichokuwepo katika gereza la Karanga na kujenga kiwanda kipya cha kisasa cha uchakataji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Ltd.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye kikao na wadau mbalimbali kabla ya kufungua kongamano la wadau wa Ngozi lililofanyika jijini Mwanza, Septemba 29,2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa na viongozi wengine wakifuatilia kongamano hilo.

Naibu katibu Mkuu wizara ya Viwanda Bw. Ludovick J. Nduhiye wa kwanza kushoto akifuatilia kongamano hilo lililofanyija jijini Mwanza, Septemba 29,2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akionyesha kiatu kilichotengenezwa na kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (KLICL) Septemba 29,2020.

Wadau mbalimbali wakifuatilia kongamano hilo lililofanyinyika jijini Mwanza, Septemba 29,2020

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Ngozi.

 

MATUKIO KATIKA PICHA