*Waahidi kuhakikisha kiwanda kinapata malighafi na masoko

*PSSSF itaendelea kutimiza wajibu wake

Na Mwandishi wetu, Moshi

Makatibu wakuu kutoka katika wizara nne wametembelea na kujionea ufungaji wa mashine katika kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro (KLICL) ukiendelea kwa kasi na kutoa wito kiwanda hicho kianze kazi kama ilivyopangwa.

Makatibu wakuu waliokuwa katika ziara hiyo ya kikazi ni pamoja na; Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bw. Andrew Massawe, Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Bw.Christopher Kadio na Naibu katibu Mkuu wizara ya Viwanda Bw. Ludovick J. Nduhiye.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bw. Andrew Massawe ambaye ndio alikuwa mwenyeji wa ziara hiyo, alisema, “Hizi ni wizara ambazo moja kwa moja zinahusika na kiwanda hiki, hivyo ili kiweze kuendelea kama ilivyokusudiwa, nimeona niwakaribishe ili kila mmoja aweze kujionea na kuweza kusaidi kuhakisha kiwanda hiki kinakuwa bora kama tunavyokusudia,”.

Bw. Massawe, alisema kulikuwa na changamoto ya malighafi haswa juu ya ubora wa ngozi ndio maana katibu Mkuu wa Mifugo amekuja na timu ya wataalam wake ili suala hili tulipatie ufumbuzi ili kiwanda hiki kiweze kuendelea vyema.

“Pia kumekuwa na changamoto ya masoko kwani kuna baadhi ya taasisi zetu za ndani hazinunui bidhaa zetu, ndio maana tunae Naibu katibu mkuu wa viwanda na Biashara ili aweze saidia katika hilo” alifafanua Bw. Massawe.

Katika kikao hicho, makatibu wakuu wote walitoa ahadi ya kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha kiwanda hicho cha bidhaa za ngozi kinazalisha bidhaa bora na ambazo zinatapata soko la ndani na nje.

Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Masoud Omari alisema ujenzi wa awamnu ya kwanza umshakamilika na ufungaji wa mitambo unaendelea na    itaanza kazi mwezi ujao mwanzoni.

“Awamu ya pili ya ujenzi inahusisha kiwanda cha kuchakata ngozi ambacho kimefikia asilimia 20 na kinatarajiwa kukamilika mwezi wa kwanza mwakani 2021. Mitambo yote imeshafika  na tunatarajia hadi kufikia mwezi wa tano mwakani 2021 usimikaji wa mitambo yote  utakuwa umekalika na baada ya hapo kiwanda kutaanza uzalishaji” alifafanua Bw. Omari.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Hosea Kashimba ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya kiwanda cha Kilimanjaro, aliwashukuru makatibu wakuu wote waliotembelea kiwanda hicho na alisema anatarajia kiwanda hicho kitaleta tija iliyokusudiwa.

PSSSF imewekeza kwenye kiwanda hicho kuitikia mwito wa serikali ya awamu ya tano ambayo ilielekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye viwanda vyenye tija kwa taifa.

PSSSF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wameingia ubia wa kuendesha mradi huo ambao ukikamilika unatarajiwa kutoa ajira kwa watanzania wapatao 3000 na kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi kwa ajili ya soko la ndani nan je ya nchi.