* Kiwanda kina maabara ya kuthibitisha ubora wa kimataifa

* Kiwanda kimechochea upatikanaji wa ajira

* Ni mkombozi kwa wakulima wa tangawizi

 Na Mwandishi Wetu

Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba, chenye uwezo wa kuzalisha tani 10 za tangawizi kwa siku ambacho ni ubia kati ya PSSSF na Chama cha Wakulima wa Tangawizi Same kinaanza uzalishaji rasmi wiki ya mwanzo wa April, 2022.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda Bw. Emmanuel Loi alipokuwa akifanya mahojiano na TBC ya kipindi maalum cha Wekeza Tanzania Wilayani Same. Bw. Lio alisema kufuatia uzalishaji wa awali na majaribio ambayo yamefanyika yametoa matokeo chanya ya mafanikio makubwa ambapo kiwanda kimeweza kuzalisha tani 10 kwa masaa 24.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba, Bw. Emmanule Loi, akitoa maelezo ya namna mashine za kuchakata tangawizi zinavyofanya kazi wakati wa ziara ya TBC ya kipindi maalum cha Wekeza Tanzania hivi karibuni.

Bw. Loi aliongeza kuwa katika kiwanda kuna maabara ya kuthibitisha ubora wa tangawizi inayochakatwa. “Ili kujiridhisha na kuhakikisha ubora tunaozungumzia kuwa ni wa uhakika, kiwanda kimewekeza kwenye vifaa vya kimataifa vya maabara vyenye ubora wa kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisisitiza Bw. Loi.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Mamba Myamba amesema kiwanda kimeajiri jumla ya wafanyakazi 24 kwa ngazi mbalimbali. Ameishukuru Serikali Kuu kwani imewasaidia wakulima kwa kuwapatia elimu ya ushirika na njia bora ya kilimo cha tangawizi kwa kutumia maafisa kilimo na biashara wa Serikali.

Wafanyakazi wa Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba wakiendelea na kazi ya kuchakata tangawizi wakati wa ziara ya TBC ya kipindi maalum cha Wekeza Tanzania hivi karibuni.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Tangawizi, Bw. Mbaraka Kibinga, alisema kwa upande wa masoko wanashirikiana na uongozi wa kiwanda kuhakikisha masoko yanapatikana “kwa sababu kwa utafiti uliofanyika   tumegundua manufaa yake katika mwili tangawizi ni zao linalohitajika kwa kwa kiwango kikubwa sana”.

Mwakilishi wa wakulima wa tangawizi, Bw. Athumani Kibacha aliishukuru PSSSF kwa uwekezaji katika zao la tangawizi kwa sababu imewapa ari ya kulima zaidi zao la tangawizi. “Uwekezaji uliofanywa na PSSSF wa kufufua Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Myamba ni mkombozi kwa wakulima kwani kumetufanya tuweze kulima kwa kujiamini kutokana  na kuwepo kwa soko la uhakika na kupanda kwa thamani ya tangawizi hivyo kuthibiti ulanguzi”.

Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba kimeundwa kwa muunganiko wa hisa za PSSSF (67%) na Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tangawizi cha Mamba (33%).

Mkulima wa tangawizi Bw. Athumani Kibacha akiteta jambo na Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Tangawizi, Bw. Mbaraka Kibinga, wakati wa ziara ya TBC ya kipindi maalum cha Wekeza Tanzania hivi karibuni.

Mfanyakazi wa Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi cha Mamba Myamba akiendelea na kazi ya kusafiisha tangawizi wakati wa ziara ya TBC ya kipindi maalum cha Wekeza Tanzania hivi karibuni.