*Yaelekeza Masoko ya uhakika yapatikane

*Yapongeza kazi nzuri inayofanyika

*Bodi yaahidi kusaka masoko zaidi

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeilekeza Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kuimarisha idara ya Utafiti na Masoko kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinapata soko la uhakika.

Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Jerry Silaa, alisema hayo wakati walipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro kwa lengo kujionea maendeleo ya uwekezaji unaoendeshwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumshi wa Umma (PSSSF) na Jeshi la Magereza.

“Bodi hakikisheni bidhaa zinapata masoko, mnasimamia ukamilishwaji wa ujenzi wa Kiwanda ili kizalishe kwa kiwango kusudiwa, kuhakikisha kunakuwepo kwa mpango wa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa wafanyakazi na kusimamia vyema mpango wa usalama kazini ili wafanyakazi wawe sehemu salama” alisisitiza Mwenyekiti wa Kamati. “Tumetembelea Kiwanda tumeona kazi zenu, mnafanya kazi nzuri, hongereni sana, kazi hii ni nzuri na ya kutolewa mfano,” alipongeza Mhe. Silaa.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na viongozi wa kiwanda cha bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro wakiwa wameshika bidhaa zinazozaliwa kiwandani hapo wakati kamati hiyo ilipotembelea kiwanda hicho.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Vijijini ambaye ni Mjumbe wa Kamati, Mheshimiwa Vuma Augustino, alisema, “Naipongeza PSSSF, huu ndio mwelekeo wa kuwa na viwanda ambavyo vitaongeza ajira kwa watanzania, endeleeni kuwa wabunifu ili mpate soko zaidi, mimi nilikuwa sijui kama kuna mambo mazuri yanafanyika hapa, jiwekeni vizuri zaidi kwenye masoko ili mjulikane”.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Lindi Mjini, Mheshimiwa Hamida Abdallah, alipongeza kazi kubwa iliyofanyika na alishauri uzalishaji usimamiwe ili bidhaa ziwe katika viwango vya kimataifa. “Hakikisheni nidhamu inakuwepo katika matumizi ya fedha. Pia ni muhimu kutoa elimu kwa wafugaji ili muweze kupata ngozi zenye kiwango kwa uzalishaji wa bidhaa bora, ” alisisitiza Mhe. Abdallah. Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Zuwena, alisema, “ Tumeshuhudia akina mama wanafanyakazi nzuri sana, tuangalie uwezekano wa kuogeza ajira kwa wanawake. Pia vijana wa Manispaa ya Moshi ambao ndio walinzi wapewe nafasi ya ajira kiwandani”.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Bw. Jerry Silaa na viongozi wengine wakiangalia moja ya hatua ya kutengeneza bidhaa za ngozi walipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Bw. Jerry Silaa, akipata maelezo kutoka kwa Bi. Jane Jaquin ambaye ni mbunifu kutoka Tsenga Prints, akieleza utaalam wa kutengeneza mikoba.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro, Injinia Masoud Omary (kulia) akitoa maelezo ya Kiwanda hicho kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, walipotembelea kiwanda hicho