Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mikoa ya kimkakati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ya Kinondoni, Ilala na Temeke iliyo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam inatoa huduma mbalimbali kwa zaidi ya wanachama 855 kwa siku.

Hayo yalibainika katika utafiti uliofanyika na Pensheni Habari katika mikoa hiyo kwa lengo la kujua huduma mbalimbali zinatolewa na ofisi hizo kwa wanachama wa Mfuko.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa mkoa wa Ilala, Bw. James Mloe alisema katika mkoa huo anahudumia wastani ya wanachama 450 hadi 500 kwa siku.

Meneja wa PSSSF, Mkoa wa Ilala BW. James Mlowe akiwa na mwanachama aliyefika ofisini kupata ufafanuzi.

“Wengi ya wanachama hao hufuatilia mafao, uhakiki wa wastaafu, michango na elimu kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea katika sekta” alifafanua Bw. Mloe.

Akizumzia jinsi wanachama wanavyofurahia huduma za Mfuko, Bw. Mlowe alisema, “Mambo mazuri ambayo wanachama wamekuwa wanavutiwa na utendaji wa mkoa na jinsi tulivyojipanga kutoa huduma, ufuatiliaji wa hoja mbalimbali za wanachama na kutoa mrejesho kwa wateja wetu.

Kwa upande wa Meneja wa Mfuko mkoa wa Kinondoni, Bi. Amina Kassimu alisema katika kuhakikisha mkoa unatoa huduma bora kwa wanachama, ofisi hiyo imekuwa na mahusiano mazuri na watendaji wa mkoa huo.

 

Meneja wa PSSSF, Mkoa wa Kinondoni Bi Amina Kassim.

“Kinondoni kwa siku tunatoa huduma kwa wanachama zaidi ya 250 na wengi hufuatilia malipo ya kuachishwa kazi, pensheni za mwezi, mapunjo, fao la elimu, mirathi, fao la kukosa ajira na fao la uzazi” alifafanua Bi. Kassimu.

Akizungumzia jinsi walivyojipanga kutoa huduma, Bi. Kassimu alisema kwa wanachama ambao hawawezi kupanda ghorofa ya kwanza zilipo ofisi za Mfuko, huwa wanahudumia wakiwa ghorofa ya chini na kwa wale ambao hawawezi kufika ofisini huwa wanafuatwa walipo hususan kwa ajili ya uhakiki.

Alisema wanachama hufurahishwa na mambo mengi ikiwemo; kulipwa stahili zao mapema na kutatua kero zao mbalimbali kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa mkoa wa Temeke, Ritha Ngalo amesema ofisi yake imejipanga vyema na kwamba ikitokea mwanachama anataka kuonana na kiongozi yeyote wa mkoa hupewa nafasi hiyo.

Lengo la kuweka mpango huo ni kuhakikisha wateja wa mkoa huo wanapata huduma bora na pia kutoa nafasi kwa viongozi kusikiliza moja kwa moja kutoka kwa wanachama hao.

Mkoa wa Temeke una jumla ya wanachama 65 ambao hawawezi kufika ofisini kutoka na sababu za kiafya, hivyo Maafisa wa Mfuko wanawajibika kwenda walipo kwa ajili ya kuwahakiki.

Meneja wa PSSSF Mkoa wa Temeke Bi. Ritha Ngallo

Bi. Ngalo alisema wanchama wengi wanaomba wajulishwe mapema juu ya tatizo lolote ili liweze kutatuliwa na mwanachama aweze kulipwa kwa wakati.

Akizungumzia uhusiano na mamlaka nyingine katika mkoa huo, Bi.Ngalo alisema, “Mahusiano na mamlaka nyingine katika mkoa yapo vyema sana, hata mkuu wa wilaya yetu ya Temeke alishawahi kututembelea kwa lengo la kuona jinsi tunavyotoa huduma kwa wateja wetu”.