Bodi ya wadhamini PSSSF yatembelea Kiwanda cha Bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro

*Waagiza kiwanda kikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia ubora

*Mitambo yote imeshawasili na kuanza kufungwa

Na Mwandishi Wetu, Moshi

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamiii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mhandisi. Musa Iyombe ametoa maelekezo kwa Menejimenti ya PSSSF pamoja wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro kuhakikisha ujenzi huo unakamalikia kwa wakati na kwa kuzingatia ubora ili kiwanda kiweze kuleta tija kwa taifa.

Mhandisi. Iyombe alisema hayo Agosti 22, 2020 mjini Moshi wakati wajumbe wa bodi ya wadhamini wa PSSSF walipotembelea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao unaendeshwa kwa pamoja kati ya Jeshi la Magereza na PSSSF.

“Tumesisitiza mambo mawili, kuhakikisha mashine tunazofungwa ziwe ambazo zimo kwenye mkataba na zifanye kazi iliyokusudiwa ili watanzania wapate kile wanachokitegemea ili tusiendelee tena kutavuta viatu na bidhaa nyingine za ngozi kutoka nje ya nchi. Pia kazi zinazofanyika pamoja na uharaka wake, ni lazima zifanywe kwa kuzingatia viwango kama ilivyo kwenye mkataba.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhandisi Masoud Omari alisema makontena 86 yenye mashine 38 za viatu na 48 za kuchakata ngozi zimeshawasili kiwandani hapo na ufungaji utachukua muda wa mwezi mmoja.

“Baada ya kufungwa kwa mashine hizo na uzalishaji ukishaanza, tunatarajia kuongezeka kwa thamani kwa bidhaa za ngozi kuanzia kwa mfugaji mpaka kwa mnunuzi, kutoa ajira kwa watakaoajiriwa na pia kutoa mafunzo katika sekta ya ngozi ambayo ilikuwa imeduamaa” alisema Mhandisi Omari.

Mhandisi Omari alisema hivi sasa wakati mradi huo wa ujenzi ukiendelea wametoa nafasi kwa vijana kutoka vyuo mbalimbali kwa ajili kupata uzoefu katika maeneo mbalimbali katika mradi huo.

Kiwanda hicho kipya kimejengwa katika eneo la hekari 25 katika gereza la Karanga katika Manispaa ya Moshi, na kikamilika kitazalisha jozi 4,000 za viatu kwa siku, soli za ina mbalimbali na bidhaa nyingine kama mikanda, mabegi, pochi, makoti, soksi za mikono na bidhaaa nyingine za ngozi na kiwanda kitatoa ajira za moja kwa moja kwa watu 3000

Mradi huo unasimamiwa na TIRDO, Chuo Kikuu cha Dar e es Salaam kupitia kitengo cha BICO na Chuo Kikuu cha Ardhi kupitia ABECC. Pia katika kundi la wataalamu inahusisha wataalam wa ndani kutoka PSSSF na Kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Karanga.